Saturday, May 18, 2013

FISI aitwae "MASIKA



                          
                                   Hadithi Ya Fisi Mvivu aitwaye Masika

Hadithi Hadithi,
Hadithi njoo, uwongo njoo, utamu kolea.
Hapo  zamani  za  kale  palikuwa  na  Fisi  aitwaye  Masika.  Masika  alikuwa  ni  Fisi  mvivu  sana  asiyependa
kufanya kazi ya aina yoyote, alipenda tu kulala muda wote. Tangia enzi zake alivyokuwa anasoma shule,
hakupenda  kukaa  darasani  na  kumsikiliza  mwalimu.  Aliwaza  tu  kurudi  nyumbani  na  kulala  kitandani
kwake.  Masika  alikuwa  ni  mvivu  kiasi  kwamba  mara  nyingine  mwalimu  wake  akifundisha  darasani,
Masika  alikuwa  akisinzia.  Mwalimu  akimuuliza  kwanini  anafanya  hivyo  alilia  kwa  sauti  ya  unyonge!
“Uuuwiii, uuuwiii, nimechoka, uuuuuwiii.” Afikapo tu nyumbani alijivuta mpaka kitandani na kulala huku
akikoroma. Wazazi wake walikuwa wakimtuma kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia lakini Masika hakuweza
kufanya hivyo kwa ajili ya uvivu wake, Masika alipenda sana kucheza tu na baadae akichoka analala bila
hata ya kuoga.



Masika aliendelea na tabia yake ya uvivu hadi ukubwani. Hakupenda kufanya kazi na alimtegemea mke
wake  ndio  afanye  kazi  na  kulisha  familia  nzima.  Kwa  kuwa mke  wake  alimpenda  sana,  alivumilia  na
kuendelea kufanya kazi  kwa bidii ili kuitunza familia. Kipindi fulani mke wake Masika aliugua ghalfa na
hali hii ilisababisha kusiwepo na chakula kabisa ndani ya nyumba yao. Mke wake akamwabia, ”mume
wangu mpendwa, jamani naomba uamke hapo kitandani ukatafute kazi ili tuweze kujipatia chakula hapa
nyumbani.”  Masika  akaijibu  kwa  uvivu  huku  akijigeuza  kitandani,  “Uuuwiii,  uuuwiii,  nimechoka,
uuuuuwiii”. Siku zilipita na wote wawili walibaki wamelala kitandani. Masika alilala kwaajili ya uzembe
wake na mke wake alilala kwa kuwa alikuwa ni mgonjwa. Baada ya siku nyingi kupita Masika aliona kuwa
mke wake haelekei kupona ilimbidi aamke na kwenda kutafuta kazi.

Punde tu Masika alivyotoka nyumbani kwake alisikia sauti ikitoka juu kwenye miti ikiita, ”Njoo, njooo,
fanya kazi upate kula”. Masika alisimama na kutazama juu ya mti nakumuona bundi mkubwa ameketi.
Bundi  huyu  alikuwa  akiitwa  Mabawa  na  alikuwa  ni  tajiri  mwenye  mashamba  makubwa  hapo  kijijini
kwao.  Alikuwa  amevaa  nguo  nzuri  zilizopendeza  na  miwani  mikubwa  aliyoitumia  kwaajili  ya  kusoma
vitabu vilivyomfundisha mengi kuhusu mambo ya dunia.  Mabawa alikuwa ni bundi mwenye roho nzuri
sana na alipenda kusaidia wanakijiji wenzake. Siku hii alikuwa amekaa juu ya mti akitafuta wafanyakazi
wa kumsaidia kuvuna shamba lake kubwa la mahindi. Masika akamwambia Mabawa, “Uuuwiii, uuuwiii,
ninanjaa,  uuuuuwiii.”  Mabawa  akamjibu,  ”  Njoo,  njoo  mwanangu,  mtu  asiye  fanya  kazi  na  asile.  Njoo

kesho asubuhi na mapema uanze kazi ili uweze kuipatia familia yako chakula”. Bwana mabawa alivyoona
hali  mbaya  ya  Masika alimuonea  huruma  akamwambia,  ”Njoo,  njoo  mwanangu,  naona  kwamba  una
njaa  sana.  Njoo  chukua  chakula  cha  kuwatosha  kwa  muda  mfupi  kisha  unaweza  kuja  kufanya  kazi
kwenye shamba langu”.

Kesho  yake  Masika  alichelewa  kuamka  kwakuwa  tabia  yake  ya  uvivu  bado  alikuwa  nayo.  Mke  wake
alijaribu sana kumuamsha mpaka alilazimika kumnyang’anya shuka lake alilokuwa amejifunikia. Masika
alijigeuza kitandani huku akilalamika kama kawaida yake, “Uuuwiii, uuuwiii, nimechoka, uuuuuwiii.”
Siku hiyo ikapita bila ya Masika kwenda kazini.

Siku  chache  zilizofuata  njaa  ilizidi  na  Masika  alishindwa  kuvumilia  akalazimika  kuamka  na  kwenda
shambani kwa bwana Mabawa. Mabawa alimkanya Masika kwa tabia yake ya uvivu lakini alimsamehe
pia. Masika alielekea shambani huku akitembea kwa kujivuta. Alifika na kukuta wenzake wameshaanza
kazi tangu mapema na waliendelea kuvuna mahindi. Alijiunga na wanfanyakazi wengine kukata mahindi,
kuyamenya,  kuyapukuchua  na  kuyajaza  kwenye  magunia  kisha  kuyapeleka  kwenye  ghala.  Ghala  hili
lilikuwa sehemu  maalum  ya  kuhifadhia  mazao  mbalimbali  kwa  ajili  ya  akiba  wakati  wa  upungufu  wa
chakula.

Pamoja  na  Masika  kupata  kazi  hii  nzuri  bado  alikuwa  ni  mvivu  kiasi  kwamba  wakati  wenzake
wameshapeleka  magunia  matatu  au  manne  yeye  alikuwa  amepeleka  moja  tu.  Kuona  hivyo  Masika
aliogopa  kuwa  bwana  Mabawa  asingemlipa  ujira  au  mshahara  uliolingana  na  wafanyakazi  wenzake.
Alifikiria jinsi ya kuweza kuongeza idadi ya magunia aliyopeleka ili yalingane na ya wafanyakazi wengine.
Alijiambia mwenyewe, ”nikisubiri wakati wafanyakazi wengine hawanioni, nitaweza kuwaibia magunia
yao na kuyakimbiza upesi ghalani. Kwa mbinu hii haitanibidii kufanya kazi nyingi lakini nitaweza kupeleka
magunia  mengi”.  Wakati  anawaza  kufanya  hivyo  bwana  Mabawa  alikuwa  akitembelea  na  kukagua
shughuli  za  kuvuna  shambani  mwake.  Masika  aliogopa  sana  alivyomuona  na  akafikiri  angeweza  hata
kupoteza kazi yake iwapo atakutwa na kosa hilo kubwa.

Akafikiria  zaidi  na  akapata  mbinu  nyingine  ya  kuongeza  idadi  ya  magunia.  Alijiambia  mwenyewe,
”Baadala ya kukata mahindi, kuyamenya, kuyapukuchua; kwanini nisichukue magunzi yaliyotoka kwenye
mahindi yaliyomenywa na wenzangu, kisha niyafunge vizuri kwenye magunia kisha niyapeleke kwenye
ghala?” Masika aliona kuwa hii ni njia nzuri sana ya kuweza kuepukana na kufanya kazi nyingi lakini bado
ataweza  kupata  ujira  sawa  na  wafanyakazi  wengine.  Basi  huku  wenzake  wakifanya  kazi  kwa  bidii  na
kujaza mahindi kwenye magunia, Masika aliwafuata nyuma na kuokota magunzi na matakataka mengine
na kuyajaza kwenye magunia yake. Alijiona mjanja sana kwa kuweza kufikiria mbinu hii ya kudanganya
na  kuonekana  kama  yeye  pia  ni  mfanyakazi  bora.  Jioni  ilipofika  magunia  yote  ya  masika  yalihesabiwa
ilimwisho wa wiki aweze kupata ujira kulingana na kazi aliyoifanya.

Siku zilipita na Masika alikuwa anaendelea kuokota magunzi na uchafu mwingine na kuyapeleka kwenye
ghala. Magunia yake yalihesabiwa kama kawaida na mwisho wa siku alienda nyumbani huku akiiwaza tu
siku ya mwisho wa mavuno ambapo atakuja kulipwa ujira wake wa wiki nzima.
Siku  ya  mwisho  ya  kazi  ya  kuvuna  ilifika  na  wafanyakazi  wote  kwenye  shamba  la  bwana  Mabawa
walikuwa  wenye  furaha  sana  kwa  kuwa  walijua  siku  hii  watalipwa  ujira  wao.  Masika  naye  alikuwa
mwenye furaha kubwa kwa kuwa mbinu yake ya kudangaya ilikuwa haijagundulika na bwana Mabawa
wala yeyote mwingine hapo shambani. Masika aliendelea siku hiyo ya mwisho kukusanya magunzi na
uchafu mwingine na kupeleka kwenye ghala.

Jioni  ilipofika  Masika  na  wanfanyakazi  wote  wengine  wakiwa  wamebeba  gunia  lao  la  mwisho,  bwana
Mabawa aliwasimamisha na kuwaeleza kuwa amefurahishwa sana na kazi nzuri walioifanya wiki nzima.
Bwana Mabawa aliwaambia, ”Asanteni sana kwa kazi yenu nzuri. Pia ninapenda kuwataarifu kuwa ujira
wenu kwa kazi zenu mzlizozifanya; Kila  mmoja wenu achukue gunia alilolibeba na mpeleke nyumbani
kwaajili ya chakula kwa familia zenu”. Masika alishikwa na mshituko mkubwa  na masikitiko kwa kuwa
alijua gunia alilolibeba lilikuwa limejaa magunzi na matakataka tu. Huku wenzake wakishangilia Masika
alianguka  chini  na  kuanza  kulia  kwa  sauti  kubwa,   “Uuuwiii,  uuuwiii,  tutakula  nini,  uuuuuwiii.” Bwana
Mabawa  alipoona  hali  hii  alimuuliza  Masika,  ”Wewe  mbona  unalia  na  hauna  raha  wakati  wenzako
wanafurahia?”  Masika  alishindwa  kumjibu  na  alibaki  tu  akiangalia  gunia  lake  hadi  bwana  Mabawa
alishawishika  kufungua  gunia  na  kuangalia  yaliyomo.  Bwana  Mabawa  alipigwa  na  butwaa  kwa  kuona
magunzi  na  uchafu  mwingine  kwenye  gunia  la  Masika.  Akamwambia  kwa  ukali,  ”Kumbe  hivi  ndivyo
ulivyokuwa  ukifanya  kila  siku!  Tabia  yako  ya  uzembe  na  uvivu  leo  imekuponza.  Kuanzia  leo  wewe  na
familia  yako  na  wajukuu  wenu  wote  na  vizazi  vyako  vyote  vinavyofuata  mtakuwa  mkila  mabaki  ya
chakula watakacho acha wengine baada ya kushiba”.

Ndio  maana  mpaka  leo  ukimtazama  fisi  utamuona  amelala  kwa  uzembe  akisubiri  wengine  kuacha  au
kudondosha chakula huku akilia ” “Uuuwiii, uuuwiii, nina njaa, uuuuuwiii.”
Hadithi yetu ya fisi mvivu aitwaye Masika ndio inaishia hapo.

hahahahhahahhahah fisiiii masikaa imeeeekulaa haahhahahha lol

>>>LEO tulikuwa na Hadithi ya FISI masika, xaxa je, Tabia hizi umeshawahi ziona????!! BADILIKA kama unazo.....comment juu ya tabia ya FISI mzembee "MASIKA"

No comments:

Post a Comment